JE WAJUA UTAJIRI UNAOMILIKI KATIKA MAISHA YAKO

Najua nimesema utajiri wengi watakua wameshtuka na kusubiri kwa hamu kuona ni utajiri gani huo.Kwa ujumla hakuna mtu asiyependa kuwa tajiri na maisha yetu kwa ujumla yametawaliwa na hamu ya kuwa matajiri kwa kuwa na umiliki wa mali nyingi sana ambazo zinaweza kumsaidia mtu kufanya kile anachokitaka kwa wakati anao utaka,ili afikie kile anachokitaka bila usumbufu wowote.
Mtu yeyote aliye na umiliki wa mali nyingi na za kutosha hupenda kujiita ama kuitwa tajiri,lakini mali hizo anazomiliki anashindwa kutambua kuwa ni vitu vinavyoweza kuisha thamani muda wowote ule(material things).Na utajiri huo ambao huyo mtu anao hutegemea kwa kiasi kikubwa utajiri wa kipekee ambao wenyewe hauhitaji nguvu ya ziada katika kuulinda isipokuwa umakini tu katika kuutumia.
Leo nataka utambue kuwa kila mtu ni tajiri,tena tajiri wa kutupwa,kila binadamu anamiliki rasilimali(resources) nyingi sana katika kichwa chake. Rasilimali hizi humzalishia faida nyingi sana ambazo huonekana na zingine zisizoonekana. Matumizi ya rasilimali hizi hayahitaji kuajiri mtu wa ziada katika usimamizi wake,isipokuwa umakini wa mtu peke yake.
Binadamu tumeumbwa sawa na kila kitu tulichonacho ni sawa hasa kwa mtazamo wa kisaikolojia,na tunatofautiana kwa kiasi chake kwa mtazamo wa kibailojia.Maana yangu ni kwamba,kwa mtazamo wa kisaikolojia ni kwamba binadamu wote tumezaliwa na kupitia hatua zilizo sawa za ukuaji na maendeleo yetu ya ukuaji ni sawa.Lakini katika hatua zote za ukuaji wa binadamu ni hatua moja tu ambayo huumpa mtu utajiri wa kudumu katika maisha yake,na hatua hii ni hatua ya ukuaji na ukomaaji wa akili(Cognitive development).Ingawa hatua hii ni endelevulakini hatua ya pekee kabisa ambayo maendeleo haya ya ukuaji na ukomaaji wa akili usipoenda na muda sahihi huweza kumletea mtu umaskini wa kudumu.

Je ni utajiri gani huo?
Hakuna utajiri wowote uliomkubwa kwa binadamu kama utajiri wa kiakili,ni changamoto nyingi sana ambazo binadamu anakutana nazo katika maisha yake lakini kwa kutokutambua rasilimali alizonazo,anashindwa kuzitumia na hatimaye kufanya maisha yake kuwa magumu na yasiyo na suluhisho.Lakini ukweli ni kwamba tunamiliki rasilimali nyingi sana ambazo zinaweza kukusaidia kupata kila kitu unachokihitaji kwa wakati wowote unaohitaji.
Wanasaikolojia wanaamini kuwa kila binadamu anamiliki rasilimali nyingi sana,na rasilimali hizo hazihusishi vitu(materials resources),isipokuwa uwezo wa kiakili(Cognitive resources). Huendelea kuamini kuwa mafanikio yoyote yanayopatika katika harakati za maisha,hutokana na rasilimali hizi za kipekee,kwani hata unaponunua gari ambalo hukuonyesha kwa watu kuwa umefanikiwa ama ni tajiri hutegemea kwa asilimia zote matumizi ya rasilimali za kiakili ambazo zimekupelekea kununua gari hilo.Mfano huo na mengine mengi ambayo hufanyika na kumuonyesha mtu kuwa amefanikiwa,hutegemea rasilimali za kiakili ambazo kila binadamu aliyepitia hatua zote za ukuaji vizuri ni lazima awe nazo.Na rasilimali hizo ninazoziongelea ambazo ni kama utajiri wa pekee alionao kila mtu ni hizi zifuatazo:
  1. Uwezo wa kufikiria; hii ni rasilimali ya pekee sana ambayo kila mtu anayeimiliki ni lazima afanikwe kwa kiasi kikubwa kwa yale anayoyatamani.
  2. Uwezo wa kutafakari; hii rasilimali ya muhimu sana ambayo husaidia kwa kiasi kikubwa kabla ya kuamua ni kitu gani unachotaka kukifanya. Hii ni rasilimali ambayo kama mtu anapungukiwa nayo huweza kufanya kile kisichotarajiwa na mwisho wake anaweza asifanikiwe.
  3. Uwezo wa kutambua; hii ni rasilimali ambayo hutegemea zaidi rasilimali zingine hasa hizo hapo juu. Uwezo huu husaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanya maamuzi sahihi kwa lipi ni lipi.
  4. Uwezo wa kufanya uamuzi; hii ni rasilimali ambayo si kila mtu anaweza kuwa nayo.Lakini ni rasilimali ya muhimu sana ambayo husaidia katika kupata mafanikio anayotamani mtu,kwani unapopungukiwa na rasilimali hii unaweza kushindwa kufanya na kupata ulichokitamani kwa muda maalumu..
  5. Uwezo wa kujenga mahusiano; ni ngumu sana kufanikiwa kama unapungukiwa rasilimali hii. Mafanikio yoyote yale hutegemea kwa kiasi kikubwa mchango wa vitu ama watu mbalimbali. Hivyo unapopungukiwa rasilimali hii unaweza kukosa hata sehemu ya kuwekeza rasilimali zako zingine ulizonazo kwa watu ama mahali pengine.
 Kama nilivyosema, na hii ni kweli kwamba kupitia rasilimali hizi ambazo ni uwezo wa kiakili,ndizo husaidia katika mafanikio yote tunayopata kwani anapopungukiwa rasilimali hata moja katika hizi unaweza kupata shida katika kukamilisha na kufikia malengo yako ili uweze kuwa mtu wa namna unayoitaka.
Tafakari na uone kama rasilimali ulizonazo zinajitosheleza?na kama hazijitoshelezi ni ipi inayopungua na utafanyaje kuipata?





Comments

Popular posts from this blog

NI NINI CHANZO CHA HASIRA

JE,WAJUA KUWA UNA TATIZO LA KISAIKOLOJIA?

NINI CHANZO CHA MIGOGORO KATIKA MAHUSIANO?