JE,WAJUA KUWA UNA TATIZO LA KISAIKOLOJIA?
Katika maisha yako ya kila siku kuna mambo mengi sana unapenda kuyafanya na pia kuona watu wengine wakiyafanya,katika hali ya kawaida ni vigumu sana kuweza kutambua kwa haraka kuwa kitu au jambo unalolifanya si la kawaida kwa sababu tu umezoea kulifanya.Katika maisha ya sasa tunayoishi na jinsi hali halisi ya maisha inavyoonekana hasa kwa nchi yetu ya Tanzania,watu wengi sana hujikuta wakifanya na wakiishi maisha ambayo hayana uhusiano halisi na jinsi mtu anavyotakiwa kuishi.
Changamoto mbalimbali za maisha pamoja na ukosefu/upungufu wa mahitaji ya msingi,ni vitu ambavyo huchangia kwa namna moja au nyingine kuwafanya watu waishi na kufanya mambo yasiyo ya kawaida na mwisho wa siku hali hii inapoendelea kumkuta huyu mtu huishia kupata matatizo ya kisaikolojia.
Matatizo ya kisaikolojia ni tabia ambazo mtu huonekana kuwa nazo zikiwa zinaambatana na dalili mbalimbali za kisaikolojia.Tabia hizi kwa kiasi kikubwa huathiri maisha ya mtu ambaye huonekana kuwa nazo.Baadhi ya tabia hizo ni kama vile upweke,msongo wa mawazo,kukosa hamu ya kufanya shughuli mbalimbali ulizozoea kuzifanya na nyingine nyingi.
Kwa siku ya leo tuangalie baadhi ya matatizo ya kisaikolojia ambayo wengi wetu tunayo, hasa wewe hapo,lakini ama kwa kutambua au kwa kutokutambua tunashindwa kuelewa tupo katika hali gani.Kama nilivyosema ni vigumu sana kwa hali ya kawaida mtu kutambua kuwa ana tatizo la kisaikolojia,hadi pale atakapo pata nafasi ya kukutana na mtaalamu wa saikolojia na akaweza kumsaidia.
Na haya ni baadhi ya matatizo ya kisaikolojia ambayo watu wengi sana tunayo,na kwa kutokutambua baadhi yetu hufurahia matendo au tabia wanazokuwa nazo ambazo ndizo hupelekea kuweza kugundulika kuwa ana matatizo hayo:
- Kulala(Sleeping Disorder):Kulala ni mojawapo ya starehe katika maisha binadamu na viumbe hai wengine,kwani kupitia kulala mtu huiruhusu akili yake kupunguzika baada ya shughuli zote alizokuwa akizifanya siku nzima,zinaweza kuwa ni za kutumia nguvu lakini pia huweza kuwa ni za kutumia akili.Kulala kunaweza kuwa ni tatizo hasa pale mtu anapolala sana katika muda usio wa kawaida,anapochelewa kulala,anapolala usingizi usio wa kawaida,anaposhindwa kupumua vizuri wakati wa kulala na pale anapokosa kabisa usingizi.Lakini pia ndoto za mara kwa mara na zisizo za kawaida ni baadhi ya dalili za kisaikolojia zinazoonyesha kuwa unaweza kuwa na tatizo la kisaikolojia.Hali hii yote usababishwa na sababu nyingi sana zikiwemo kuwa na msongo wa mawazo(stress),hali ya wasiwasi juu ya jambo au hali inayoweza kukutokea,uanzaji au utumiaji uliopitiliza wa vilevi(substance use) pamoja na sababu nyingine nyingi.
- Wasiwasi uliopitiliza(Anxiety Disorder):Katika hali ya kawaida ya maisha kila kiumbe aliye hai hupatwa na wasiwasi,na wasiwasi huu umpelekea mtu kuwa na hali ya uwoga.Uwoga ni kinga, husaidia na wakati mwingine huepusha mambo mengi.Lakini uwoga uliopitiliza kiwango hilo huweza kuwa ni tatizo.Hakuna kitu ambacho hufanyika ama hutokea bila sababu,na vivyo hivyo uwoga humtokea mtu kwa sababu maalumu.Na hapo ndipo tunapata aina tofauti za uwoga; uwoga wa vitu,uwoga wa hali tunazokutana nazo,uwoga kutokana na mazingira,uwoga wa watu na pia kuna uwoga kutokana na matukio yaliyopita.Hapa ndipo kila mtu huwa na eneo lake la kujidai ambalo kwa namna moja ama nyingine humfanya kukosa amani ya kukamilisha malengo yake kwa wakati.
- Kubadilika kwa hali (mood) mara kwa mara(Bipolar Disorder): Katika maisha ya kila siku tunakutana na mambo mbalimbali ambayo huweza kukufanya kuwa na furaha sana,lakini mambo mengine huweza kukufanya kukosa furaha kabisa na kuyaona maisha yako yapo katika sayari tofauti.Mtu anapokuwa na furaha ya mara kwa mara na inayopitiliza kiasi huweza kuwa na tatizo la kisaikolojia,kwani kupitia furaha hiyo huweza kujikuta akifanya mambo yasiyo ya kawaida na ambayo hayajazoeleka na kumfanya kuonekana wa ajabu sana. Baadhi ya mambo hayo ni kama kukosa usingizi,kufanya maamuzi bila kujali madhara yake pamoja na nyingine nyingi.Lakini pia huzuni ni kitu cha kawaida hasa pale unapokuwa umekutana na kitu ambacho hukukitegemea,lakini huzuni iliyopitiliza sana huweza kuwa na tatizo la kisaikolojia.Mtu aliye na huzuni iliyopitiliza mara nyingi hujiona mpweke sana,na mwisho wake huishia kuwaza mawazo yasiyo ya kawaida kama vile kujidhuru na hata kuwadhuru wengine. Mtu huyu huishia kulia mara kwa mara na kuwa na mtazamo hasi wa maisha yake kila siku na kwa kila analolifanya.
- Kukosa/kupungukiwa umakini katika utendaji na utekelezaji(Attention Deficit Disorder): Hii ni hali ambayo kwa kipindi cha nyuma ilikuwa ikiwakuta kwa kiasi kikubwa watoto wadogo kutokana na umri pamoja na malezi wanayopata.Lakini tatizo hili kwa sasa husumbua watu wa rika zote bila kujalisha ni umri gani,tatizo huwa nalo mtu lakini kwa yeye kutokutambua hujikuta akipata lawama kila wakati kutoka kwa ndugu,jamaa,marafiki na hata watu unaofanya nao shughuli zako za kila siku.Ukiona unapata lawama za mara kwa mara na kujikuta unashindwa kupangilia,kutekeleza na kukamilisha majukumu yako kiuhakika na inavyotakiwa,ama unakua unakosa uamuzi sahihi wa nini ufanye na nini uache,tambua unaweza kuwa na tatizo la kisaikolojia.
- Kupenda ama kutokupenda kula(Eating Disoder): Hili ni tatizo ambalo kwa mazingira ya kawaida ni vigumu mtu kutambua kuwa ana tatizo la kisaikolojia linaloendana na kupenda ama kutokupenda kula.Kama yalivyo matatizo mengine kwa kuwa na ugumu wa kutambua,vivyo hivyo tatizo hili huwa na ugumu huo.Si kwamba kila mtu anapopenda kula sana ana njaa ama la,lakini pia si kila mtu ambaye hapendi kula hana njaa ama ni mvivu wa kula. Lakini kuna sababu za kisaikolojia ambazo huweza kwa kiasi kikubwa kumsababishia mtu kuwa katika hali hiyo.Baadhi ya sababu hizo huweza kuwa msongo wa mawazo(stress),hali ya wasiwasi iliyopitiliza(anxiety),na sababu nyingine nyingi.Utafiti unaonyesha kuwa wanawake ndio huathiriwa zaidi na tatizo hili kuliko wanaume,na hii ni kutokana na aina ya maisha wanayoishi.Lakini pia wanaume hupatwa na tatizo hili kwa kiasi kidog kuliko wanawake.
- Tabia na hisia binafsi(Personality Disorder):Kila binadamu ana tabia na hisia zake binafsi juu ya kila kitu na kila hali anayokutana nayo katika maisha yake ya kila siku.Tabia kuu ya binadamu ni kuwa na imani juu ya kila kitu anachokifanya kuwa ni sahihi kwake kutegemeana na hisia zake zinavyomtuma juu ya jambo hilo,na kumbadilisha mtu tabia aliyonayo si jambo rahisi sana kama tunavyofikiria.Lakini pia hata kumbadilisha mtu hisia zake juu ya jambo fulani au hali fulani pia si kazi rahis kama tunavyofikiria.Ni vigumu sana kwa mtu kujitambua kuwa ana matatizo ya kisaikolojia yanatokana na tabia zake ama hisia zake juu ya vitu mbalimbali,ispokuwa pale anapowea kuambiwa na mtaalam wa saikolojia na ushauri.Baadhi ya dalili za kisaikolojia ambazo huonekana kwa mtu mwenye tatizo hili ni pamoja na kukosa uwezo wa kuwasiliana na watu wa aina tofauti na aliowazoea(interpersonal functioning),kushinndwa kuzuia misukumo mbalimbali ya kufanya vitu(control impulses) pamoja na nyingine nyingi.Mtu huweza kutambulika kuwa ana tatizo la kisaikolojia linalotokana na tabia binafsi pamoja na hisia pale tu ambapo tabia hizo humzuia kufanya pamoja na kushirikiana na jamii katika mambo tofauti tofauti.
Haya ni baadhi tu kati ya matatizo mengi ya kisaikolojia ambayo watu wengi sana tunayo,lakini kwa kutokujua kutokana na hali pamoja na mazingira tunamoishi ni vigumu sana kuyatambua.Lakini unapogundua kuwa una dalili za tofauti na hali halisi ya tabia za kawaida ni lazima ujiulize na kama ikiwezekana tafuta mtu anayeweza ukusaidia kutambua hali hiyo.
Kumbuka: Si kila hali isiyo ya kawaida inapokutokea ni tatizo la kisaikolojia,isipokuwa pale tu linapoonekana kuwa na dalili za kisaikolojia.Na dalili za kisaikilojia huonekana pale unapojigundua kuwa na tabia zisizo za kawaida na ambazo hazijazoeleka katika jamii(abnormal behaviors),sikiliza watu wanavyosema juu ya tabia zako mara kwa mara,na utambue zipo katika mlengo gani.Kisha chukua hatua.
************************
KWA LEO TUISHIE HAPO LAKINI ENDELEA KUFUATILIA MADA HII KIPINDI KINGINE UWEZE KUELEWA,NAWE UNAWEZA KUWA NA TATIZO LA KISAIKOLOJIA PIA BILA KUJITAMBUA.
Kama una swali lolote ama unataka kujua zaidi juu ya chochote ama ushauri juu ya nini cha kufanya kama,acha comment yako hapo chini ama unaweza kunitafuta kwa anuni zilizopo hapo juu
LOADING.....................
Comments
Post a Comment